Serikali imekitaka Chuo cha Kodi (ITA), kuimarisha mafunzo yanayolenga kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kubaini na kusimamia kodi zinazotokana na biashara za mtandaoni, huku kikitakiwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI).
Wito huo umetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, wakati wa Mahafali ya 19 ya Chuo cha Kodi yaliyofanyika katika Chuo hicho jijini Dar Es Salaam.
Alisema mabadiliko ya kiuchumi duniani na kukua kwa biashara za kidijitali kunahitaji uwepo wa wataalamu wenye ujuzi wa kutambua na kusimamia vyanzo vipya vya mapato ya kodi.
“Tunahitaji wataalam wa kuchambua na kubaini kodi katika biashara za mtandaoni ambazo zinazidi kuongezeka kila siku. Pia tunahitaji wataalam wa kutunga sera za kodi ambazo zinaendana na uchumi wa sasa,” alisema CPA Mkude
Amesisitiza kuwa Chuo cha Kodi kinapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuandaa wataalamu hao ili kukidhi mahitaji ya uchumi unaobadilika na kuimarisha usimamizi wa kodi nchini.
Katika hatua nyingine ameitaka Menejimenti ya Chuo kuhakikisha upanuzi wa programu za masomo, hususan katika ngazi ya uzamili, unaenda sambamba na ubora wa mafunzo na mahitaji halisi ya biashara za kimataifa pamoja na mifumo ya utozaji kodi duniani.
Alisema Serikali itaendelea kukiwezesha Chuo hicho kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kiendelee kutoa wataalamu wa forodha na kodi watakaosaidia kuboresha sera na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
CPA Mkude, amekitaka Chuo hicho kuongeza tafiti zinazolenga kutatua changamoto za mfumo wa kodi nchini, hususan kupanua wigo wa kodi, kurahisisha ulipaji kodi na kuongeza ari ya wananchi kulipa kodi kwa hiari.
“Serikali inapenda kuona changamoto zilizopo katika sera na mfumo wa kodi zinapatiwa ufumbuzi na makusanyo ya mapato yanaongezeka pamoja na kuongezeka kwa ulipaji kodi wa hiari” alisema CPA Mkude
Alibainisha kuwa Tahiti hizo zinapaswa kusaidia nchi kuwa na sera za kodi zenye ufanisi, haki na usawa, huku akibainisha kuwa Wizara ya Fedha ipo tayari kushirikiana na Chuo hicho katika kuwawezesha watafiti na kubaini maeneo muhimu ya kufanyia tafiti.
Akihusisha jukumu la TRA na mipango ya maendeleo ya Taifa, amesema Mamlaka hiyo ina nafasi muhimu katika kuchangia utekelezaji wa Dira 2050, ambayo ina nguzo kuu tatu, mojawapo ikiwa ni uchumi imara na shindani.
Amesema Chuo cha Kodi, kama sehemu ya TRA, kina wajibu wa kutoa mapendekezo na ushauri wa kitaalamu kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikia matarajio ya wananchi kupitia Dira hiyo.
Aliwapongeza wahitimu hao na kuwataka kutumia elimu waliyoipata kujiendeleza kitaaluma, kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa kodi na kujifunza kila mara ili kukabiliana na mabadiliko ya ulimwengu wa kazi.
Aidha, amewahimiza wahitimu kutumia elimu yao siyo tu kutafuta ajira, bali pia kuanzisha shughuli za kiuchumi na kutoa huduma kwa uadilifu.
“Uadilifu utawa jengea heshima na kuwapa fursa ya kukua katika shughuli zenu,” alisema CPA Mkude
Kwa upande wake Kamishna Mkuu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), CPA. Yusuph Juma Mwenda, alisema Chuo hicho kinaendelea kutoa mchango mkubwa kwa TRA kwa kuendelea kuzalisha wataalamu mbalimbali wakiwemo wataalamu wa Kodi, jambo linaloisaidia Mamalaka hiyo kuendelea kuongeza makusanyo ya pato.
Chuo cha Kodi (ITA) kimeanzisha programu mbili mpya za Shahada za Uzamili katika Kodi (Master of Taxation) na Forodha na Biashara ya Kimataifa (Master of Customs and International Trade), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza wataalamu wenye ujuzi na maarifa ya kina katika sekta za kodi, forodha na biashara ya kimataifa ambapo Programu hizo zimezinduliwa rasmi Novemba 27, 2026 na Mhasibu Mkuu wa Serikali CPA. Leonard Mkude.
‘’Uanzishwaji wa programu hizo umetokana na mahitaji yanayoongezeka ya wataalamu katika maeneo ya kodi, forodha na biashara ya kimataifa, sambamba na azma ya kuimarisha elimu ya juu, kukuza utaalamu na kujenga uwezo wa kitaifa katika sekta hizo muhimu kwa maendeleo ya Taifa’’ alisema CPA. Mwenda.
Alisema Shahada ya Uzamili katika Kodi inalenga kuwaandaa wataalamu watakaosaidia kuboresha sera na mifumo ya kodi, kupanua wigo wa kodi, kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuimarisha ulipaji kodi wa hiari.
Aidha, wahitimu wa programu hiyo wanatarajiwa kuwa na mchango katika kubuni mifumo ya kodi inayovutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kwa upande mwingine, Shahada ya Uzamili katika Forodha na Biashara ya Kimataifa inalenga kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kurahisisha biashara, kuimarisha usimamizi wa forodha na mipaka, kuongeza ufanisi wa taratibu za biashara na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Amesema Uzinduzi wa programu hizo ni hatua muhimu katika uwekezaji wa kimkakati wa rasilimali watu, kwa kuwa unatoa fursa ya kupata elimu ya juu na utaalamu utakaosaidia kuchochea mageuzi katika usimamizi wa kodi, forodha na biashara ya kimataifa.
Aidha, amesema programu hizo zinatarajiwa kuwa na mchango katika kuimarisha mapato ya Serikali, kukuza biashara na uwekezaji pamoja na kuunga mkono utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya Taifa kuelekea Dira 2050.
Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 743 waliohitimu masomo katika mwaka wa masomo 2025/2026 walitunukiwa vyeti katika ngazi za Astashahada, Stashahada, Shahada na Astashahada ya Uzamili.
