Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema kuwa Tanzania imepokea na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Kituo cha Maendeleo cha Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo-OECD), ambacho kimeishauri nchi ijiunge na Kituo hicho ili iweze kunufaika na huduma kinazotoa ikiwemo kufanya utafiti utakaosaidia kukuza zaidi uchumi wa Taifa kupitia uboreshaji wa mifumo ya kodi.
Mhe. Balozi Omar amesema hayo Jijini Paris nchini Ufaransa baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Kituo hucho ukiongozwa na Mkurugenzi wake Mtendaji, Bi. Ragnheidur Elín Árnadóttir (Ragga), Kando ya Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi kwa ajili ya Afrika, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha OECD.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Shirika hilo la kimataifa ili kuchochea maendeleo ya nchi ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho cha OECD alimkabidhi Mhe. Waziri wa Fedha Ripoti ya Utafiti wa Kiuchumi kwa baadhi ya nchi za Afrika.
Katika kikao hicho, pande zote mbili zimejadili umuhimu wa kubadilishana takwimu za kodi kwa ajili ya ulinganisho wa mifumo ya kiuchumi ambapo Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na OECD katika kuimarisha utafiti wa mifumo ya ukusanyaji kodi na uwekezaji
Mkurugenzi Mtendaji wa OECD, Bi. Ragnheidur Elín Árnadóttir (Ragga), walielezea utayari wao wa kuisaidia Tanzania, endapo itajiunga na Kituo hicho, katika kufanya tafiti za mabadiliko ya uzalishaji, ikiwemo matumizi ya teknolojia, akili Unde, na uwekezaji katika miundombinu.
OECD ni Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (Organisation for Economic Co-operation and Development), likiwa na nchiwanachama 38, ikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Marekani, Japani, Uingereza, Mexico, Chile, na nyingine nyingi.
Kazi zake kuu ni kuchambua sera za kiuchumi na kijamii, kutoa takwimu na utafiti, na kutoa mapendekezo kwa serikali za nchi wanachama kuhusu mambo kama kodi, elimu, afya, biashara, mazingira na maendeleo. Mara nyingi huitwa “klabu ya nchi zilizoendelea,” ingawa kwa sasa inajumuisha nchi zenye viwango tofauti vya uchumi.


