Uongozi wa klabu ya Atlético Madrid umetishia kuifikisha mahakamani miamba ya soka nchini Hispania, Barcelona, kufuatia mzozo unaomuhusu mshambuliaji wao, Julián Alvarez. Hatua hii imekuja mara baada ya Alvarez kutoa kauli iliyoashiria kutaka kuondoka akisema: “Kitu bora zaidi ni kuomdoka Atlético Madrid, nataka kutimiza ndoto yangu.”
Atlético imechukizwa na vitendo vya Barcelona kuingia kwenye mazungumzo na mchezaji huyo kinyume cha taratibu wakati bado ana mkataba. Chanzo cha ndani kutoka Atlético kimeiambia Diario AS:
> “Nafasi ya mchezaji huyu kuuzwa Barcelona ni sifuri. Hakuna kiasi cha fedha ambacho Barcelona wanaweza kulipa kwa ajili ya Julián, na hatohamishiwa kwenda huko. Ama walipe kifungu cha dharura cha pauni milioni 500 (€500M) au hakuna biashara.”
Klabu hiyo inapanga kuwasilisha malalamiko rasmi mbele ya chombo cha sheria cha michezo cha FIFA dhidi ya Barcelona. Chanzo hicho kiliongeza kuwa:
> “Kila mtu anajua kuwa hiyo ni klabu isiyo na uaminifu. Lakini safari hii wamekutana na klabu, Atlético de Madrid, ambayo haitawafanya waondoke na ushindi hivi hivi.”
