
Denis Mpagaze
______________________
1. Wakati sisi tunafarijiana kwamba kufeli ni sehemu ya maisha, kwa Donald Trump kufeli ni dhambi kubwa
2. Anachojua yeye ni wa kushinda tu! Hata aliposhindwa Urais wa Marekani kipindi kile alisema hajashindwa ila aliibiwa kura.
3. Jamaa ni kingβangβanizi wa kushinda. Afe kipa, afe beki, ushindi kwake ni lazima. Daima mbele, nyuma mwiko.
4. Wakati wa kampeni alikoswakoswa kufa kwa risasi lakini kesho yake tulimuona majukwaani akiomba kura.
5. Alipambana mwanzo mwisho kama Mwabukusi. Leo ni Rais wa wa 47 wa Marekani. Cheers Trump!
6. Tabia yake ya kutoamini katika kufeli ndo humfanya kila anapoanguaka aweze kuinuka tena kwa kishindo.
7. Trump amewahi kufilisika kwenye biashara zake mara kadhaa hadi watu wakasema Trump amekwisha lakini bado aliinuka. Wengi wakifilisika wanapitilizaga. Hawarudigi! Tunawajua.
8. Trump kupitia Kitabu chake cha “The Art of the Deal” anasema “Mwenye nia njema huwa hakati tamaa”. Hii nimeipenda! Wewe je?
9. Ila tuacheni matani Mchizi maisha anayajua na kupambana ana jua vilevile.
10. Labda nikwambie tu, hili dingi hesabu zake huwa sio za kuangalizia. Hili ni jeshi la mtu mmoja.
11. Kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa hili jitu ndiyo maana nimeamua kukuletea historia yake.
12. Kupitia historia ya Trump nimejifunza kwamba, historia ya mtu ina mchango mkubwa katika kutoboa kimaisha au kutoboka kimaisha!
13. Jitahidi kuandika historia yako vizuri ili usiwape shida watoto na wajukuu zako! Babu yake Trump aliandika historia yake vizuri, leo mjukuu wake ni Rais wa Taifa Kubwa Duniani; Taifa ambalo likipiga chafya dunia nzima inapata mafua.
14. Mafanikio ya Donald Trump yameanzia kwa babu yake Frederick Trump ambaye alikuwa mfanyabiashara mwenye asili ya Kijerumani.
15. Kwa sababu za kiafya Babu alikimbilia Marekani ili kukwepa kuingia jeshini. Aliingia Marekani mwaka 1885 akiwa mtoto wa miaka 16.
16. Marekani alianza kujitafutia mkate wa kila siku kupitia unyoaji, wakati huo tunanyoa kwa mikasi.
17. Kutokana na kazi ya kunyoa, alianza kuwekeza katika migahawa, madini, grosari, makasino, majumba na ardhi pia. Mpaka huyo babu anakufa tayari alikuwa milionea. Aliacha utajiri wa $31,359 sawa na $ 400,000 kwa sasa.
18. Mke wake Elisabeth na Mwanaye Fred waliendeleza utajiri wake, hawakuuza kama wafanyavyo wajinga
19. Fredrick ndiyo baba wa Donald Trump. Alizaliwa mwaka 1905. Huyu ndo alipokea kijiti cha utajiri kutoka kwa Babu, akakimbia nacho, akampasia Donald Trump.
20. Hapa ndo uelewe kuna watu wamezaliwa wanavikuta. Trump anavimba kupitia biashara aliyoanza babu mpaka mjukuu.
21. Wazungu na wahindi wanautamaduni wa kuendeleza mali za familia. Sisi hivyo havipo. Huku kwetu ukiona mtu katoboa basi ni juhudi zake, ndiyo maana matajiri wetu wanakuwa wakuda sana kwa ndugu na Watoto wao. Hakuna kugusa mali.
22. Alichofanya Trump katika utajiri wa familia ni kufanya kazi kwa bidii kuupanua zaidi. Analala masaa manne tu.
23. Mpaka sasa utajiri wake umelala kwenye zaidi ya vyanzo 50 ya mapato.
24. Mwamba ana majengo makubwa, hoteli na bado anaendelea kujenga manjengo mengine ya kifahari kama vile Trump Place,Trump World Tower, Trump International Hotel and Tower na mengine kibao. Ana mijengo mpaka Mumbai, Instabul na Ufilipino.
25. Lakini pia amewekeza sana kwenye ulimwengu wa burudani na huu ndiyo umempa umaarufu mkubwa duniani. Amekuwa mmiliki wa shindano la Miss Universe, Miss USA, na Miss Teen USA. Alikuwa na kipindi maarufu cha TV kilichompa umaarufu mkubwa duniani.
26. Kiliitwa The Apprentice. Yupo pia katika fasheni, kasino na mieleka.
27. Anamiliki biashara za fanicha, vyakula, maji ya kunywa, tai za shingoni na vyuo vya ujasiriamali. Kuwa na chanzo kimoja cha mapato kama figo ni hatari.Kikifa unakufa!
28. Lakini pia Trump ni mwandishi wa vitabu na kupitia uandishi huo anapiga pesa nyingi tu.
29. Anasema Role Model wake ni Baba yake Mzazi. Trump anabidii mpaka kwenye kutukana.
30. *Mzee anatukana sana sijawahi kuona. Akikutukana habakizi neno. Ana vijembe mndengereko na mzaramo wakasome. Huu utukutu wake hajaanza leo.*
31. Alizaliwa hivyo ndiyo maana alipofikisha umri wa miaka 13 walimpeleka kusomea shule ya kijeshi maana ndo waliomuweza. Amesoma pale Kew β Forest School.
32. Mwaka 1964 alijiunga na Chuo Kikuu cha Fordham na baadaye Wharton School, Pennsylvani University alikopata Digrii yake ya Uchumi.
33. Akiwa chuoni alifanya kazi kwenye kampuni ya familia yao ya Elizabeth Trump & Son. Uzuri wa nchi za mbele, mtu unasoma na bado unaweza kufanya kazi na kupiga hela. Hausomi kinyonge na kupauka sana kama huku.
34. Trump ana pesa lakini hanywi pombe wala hali fegi kitu ambacho ni nadra sana kwa watu wenye pesa. Ila sasa kilevi chake kikubwa ni mademu.
35. Anapenda sana walimbwende, hata wake zake wote anachomoaga kwenye ulimbwende.
36. Pamoja na uchekibobu wake wote huo walau huwa anamtaja taja Mungu ndiyo maana Bishop Gwaji wa Tanzania anamkubali. Chawa wake walipomwambia wewe ndiyo mtu maarufu duniani kwa sasa, alikataa na kuwaambia βMtu Maarufu Duniani ni Yesu Kristo.β
37. Mwaka 2019 alimchagua Mchungaji wake Binafsi Paula White kuwa Afisa Mahusiano wa White House.
38. Juzi nimemskinia anasema jinsia pekee zinazotambuliwa na Serikali ya Marekani ni wanaume na wanawake, na watatambuliwa wakati wa kuzaliwa. Hapa amenikosha.
39. Mkristo wa kweli hawezi ruhusu huu upuuzi uliokatazwa kwenye Biblia. Sasa anakwambia anataka kurudisha Biblia Marekani.
40. Amegundua Marekani mambo yanaenda mlama kwa sababu wamemsahau Mungu!
41. Trump ni Mkristo aliyeweka rekodi ya kufunga ndoa na kuvunja ndoa kabla ya kifo. Hapa Mzee alizingua. Halafu Jamaa akivunja ndoa hanaga bifu na x wake kama tunavyofanya sisi.
42. Kuna siku alisupport harusi ya x wake kiroho safi. Wewe kuweza? Huyo x ndo alikuwa mke wake wa kwanza. Aliitwa Ivana Zelnickova.
43. Ivana aliolewa na Trump baada ya kuachika. Alifunga ndoa na Trump mwaka 1977, wakazaa watoto watatu, Donald Jr (1977), Ivanka (1981), na Eric (1984).
44. Mwaka 1990 ndoa ikavunjika. Mwakan1995 akaolewa tena! Mwaka 1997 ndoa ikavunjika. Mwaka huohuo Ivana akaingia kwenye mahusiano. Mwaka 2005 kabla hawajafunga ndoa mwanaume akafa.
45. Mwaka 2008, Ivana akafunga ndoa na kijana wa miaka 36 na wakati yeye anamiaka 56. Lishangazi ndani ya ndoa.
46. Kwenye hii ndoa sasa Donald Trump ndo alisponsor. Ilikuwa kufuru. Ilikula bilioni 7 za Tanzania.
47. Baada ya mwaka mmoja ndoa ikavunjika. Mama hakuwa na nyota ya kudumu kwenye ndoa. Mwaka.2022, Ivana akiwa na umri wa miaka 73 alifariki dunia. Acha apumzike tu maana siyo kwa hekaheka zile.
48. Sasa tuendelee na ndoa za Trump. Baada ya ndoa yake ya kwanza kuvunjika kwa sababu ya mchepuko wake Maria Maples, ilibidi tu mchepuko awe mke. Wakapata mtoto mmoja, anaitwa Tiffany Aliana Trump. Baada ya miaka sita ndoa ikavunjika.
49. Mwaka 2005 alimuoa Mlimbwende Slovenia Melania Knauss. Wana mtoto mmoja wa kiume, anaitwa Barron. Sasa Trump ni babu wa wajukuu kumi na bado yuko strong.
50. Halafu hafanyi mazoezi kabisa. Anasema kufanya mazoezi kunapunguza nguvu iliyoko mwilini. Mwili huwa unajichaji.
51. Trump ni mtu anayejipenda sana na kujikubali kupita maelezo. Disemba 2015 Daktari wake binafsi alitoa ripoti ikisema Trump ndiye mtia nia wa urais mwenye afya bora kuwahi kutokea nchini Amerika. Miaka mitatu baadaye yaani 2018 daktari yuleyule aliyetoa ripoti kuhusu afya yake alisema ripoti ile ya awali Trump ndiye alisema iandikwe vile.
52. Trump bhana. Aliwahi kusema pia duniani kuna vitabu bora viwili tu, cha kwanza ni Bibilia na cha pili ni kitabu alichoandika yeye, kinaitwa βArt of the Deal.β
53. Huyu ndiyo Rais Donald Trump, kiumbe ambaye akitaka kitu lazima atapambana mpaka atakipata haijalishi ni lini.
54. Ndoto yake ya kuutaka urais ilianza mwaka 1987, akaja kuupata kwa mara ya kwanza 2016 na 2024 tena. Aliingia kwenye siasa kwa lengo la kupata urais na siyo itikadi ndiyo maana alikuwa anahama hama vyama.
55. Alijiunga na Republican mwaka 1987, ila akaona upepo wa kupata Urais hausomi. Akahamia Reform Party mwaka 1999. Huko akapata kaupenyo. Mwaka 2000 akajaribu urais akadunda.
56. Mwaka 2001 akahamia Democratic. Huko akaona ndiyo kabisa Demokratic inawenyewe na wenyewe ni sisi, hapa nalamba Koker. Mwaka 2009 akarudi Republican na hatimaye akapata Urais. Unaona hesabu hizo?
57. Kabla ya kugombea Urais alifanya utafiti kwanza aone kama anatosha. Alitumia zaidi ya bilioni mbili za Kitanzania. Matokeo yakamuonyesha anaweza. Siyo mwenzangu unakurupuka tu kwenda kuchukua fomu kwa sababu washabiki zako wa mitandaoni wamekwambia unaweza. Nenda kwenye ground ukaone maajabu. Mitandao inazingua nyie!
58. Basi bwana! Oktoba 2013 chama chake cha Republican kilimpendekeza kugombea Ugavana katika jimbo la New York akakataa, yeye akasema hivyo siyo viwango vyake.
59. Viwango vyake ni Urais. Habari za kuanzia chini mtajua wenyewe. Tatizo la kuanzia chini unaweza kubaki hukohuko chini.
60. Juni 16, 2015 Trump akatangaza rasmi nia ya kugombea urais wa Marekani. Matangazo haya yaliruka moja kwa moja kutoka kwenye jengo lake la kifahari la Trump Tower jijini Manhattan akitamba na kaulimbiu yake ya MAKE AMERICA GREAT AGAIN.
61. Alitangaza kujifadhili kwenye kampeni zake zote ili kuepuka kupangiwa.
62. Trump alipoonyesha nia ya urais, wakuda wake wakaanza kufukua makaburi ya tangu miaka ya 2005.
63. Rekodi zake za manyanyaso kwa wanawake zikamwagwa hadharani. Watu wa chama chake wakababaika. Wakajua hapa tunapigwa. Mwamba hata hakutetereka. Aliforce mpaka kikaeleweka. Akawa Rais.
64. Walichuana vikali na Hillary Clinton, mwana mama aliyekuwa na uzoefu mkubwa sana katika siasa.
65. Sera zake zilizua taharuki na hasira kwa wengi, wakamuita mbaguzi wa rangi, wengine wakamuita punguani lakini hakubadilisha mitazamo yake.
66. Aliwakomalia sana watu kutoka nchi za kiislamu na Mexico. Alisema Mexico ndo wanaleta dawa za kulevya Marekani na vibaka. Atajenga ukuta. Na kweli alipopata Urais alijenga ukuta.
67. Wakati wa kampeni zake Trump aliweka hadharani utajiri na mali anazomiliki, lakini aligoma kutoa hadharani rekodi ya kodi.
68. Walipozidi kumshinikiza aliwaambia taarifa za kodi zake haziwahusu,watafute kazi nyingine za kufanya na yeye ataendelea kila siku kutafuta njia za kulipa kodi ndogo kadiri awezavyo.
69. Novemba 8, 2016 Trump alishinda kiti cha Urais na kuapishwa Januari 20, 2017, akaandika historia ya kuwa Rais wa kwanza wa Marekani ambaye hajapitia jeshini na Rais wala hajawahi kushika wadhifa wowote serikalini.
70. Hakuwahi hata kuwa mwenyekiti wa Kijiji. Hakuwa na uzoefu wa siasa. Aliamini uzoefu utamkuta kazini.
71. Alitawala kwa shida sana. Alikosolewa na kushambuliwa sana. Mwamba hakusikiliza kelele za watu. Aliwahi kuwaambia haters wake kwamba mnanichukia kwa sababu mnajua nawazidi akili.
72. Marekani walimchoka mpaka akapoteza kiti cha Urais. Rais Biden akachukua nchi.
73. Tangu apoteze urais wake Donald Trump hakuwahi kupoa. Amemsumbua sana Biden. Alijipanga upya. Juzi wameingia kwenye kinyangβanyiro akashinda.
74. Sasa mwamba ndiyo Rais wa 47 wa Marekani. Kaweka rekodi ya Rais wa pili kuingia madarakani kwa vipindi viwili tofauti. Wa kwanza alikuwa Grover Cleveland miaka 132 iliyopita.
75. Trump sasa ni babu wa miaka 78. Alizaliwa mwaka 1946.



