
LIVERPOOL, ENGLAND. ROBERT Firmino ameamua kuondoka Liverpool bure mwisho wa msimu huu baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka minane akishinda mataji saba.
straika huyo ameamua pamoja na familia yake kuwa hataikubali ofa aliyowekewa mezani na Liverpool ya kumtaka aendelee kukiwasha Anfield na kwamba ataondoka mwezi Julai.
Firmino, 31, anajivunia uhusiano wake na Liverpool, klabu, kocha, wachezaji wenzake na wafanyakazi wote – lakini anataka kujaribu changamoto mpya kama ilivyobainishwa na Skysports.
Kocha Jurgen Klopp na bodi ya Liverpool wamefahamishwa kwamba straika huyo atatoa mkono wa kwaheri ndani ya miezi michache ijayo.

Bobby alicheza kwa kiwango cha juu Liverpool na kuiwezesha kushinda mataji mbalimbali ikiwamo kubeba ubingwa wao wa kwanza wa Ligi Kuu England waliousotea kwa miaka 30 na pia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mataji aliyoshinda akiwa na Majogoo hao ni Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu England, UEFA Super Cup, Kombe la Dunia la Klabu la FIFA, Kombe la FA, Kombe la Carabao na Ngao ya Jamii.



