
. Watu tisa wakiwemo viongozi wa kisiasa wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kulima bangi katika eneo la msitu wa hifadhi ya Mienze iliyopo kijiji cha Wavu kata ya Shabaka wilayani humo.
Watu hao wamekamatwa kufuatia operesheni inayofanywa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Grace Kingalame kwa kushirikiana na jeshi la polisi pamoja na idara ya misitu ambapo tayari mashamba yenye hekari zaidi ya sita yaliyolimwa bangi yameteketezwa.
Akizungumza wakati wa uteketezwaji wa mihadarati hiyo mkuu huyo wa Wilaya amesema hayupo tayari kuona baadhi ya watu wakifanya biashara ya kulima bangi wilayani humo na kuwataka wenye tabia hiyo kuacha mara moja.
“Wanaofanya biashara ya kulima bhangi watafute pakwenda mimi kama mkuu wa wilaya sipo tayari kuona jamii ya Nyang’hwale wanakuwa kwenye hali hatarishi kwa sababu ya mihadarati nawasihi sana tufanye kazi za maendeleo.“ alisema Kingalame na kuongeza,
“Nimetumwa na Rais kuhakikisha maendeleo yanasonga mbele kwa ambao watatupinga wakidhani wanaweza kufanya shughuli za kihalifu ikiwemo hii ya kupanmda bangi waache.”
Aidha amewataka watendaji wa vijiji kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama na kuwataka kutoa taarifa mapema pindi wanaopoona viashiria vyovyote vya uhalifu.
Afisa misitu wa Wilaya hiyo, Asafu Manya amesema taarifa za uwepo wa mashamba katikati ya msitu huo zimetolewa na wasamaria wema na kuitaka jamii kuacha kuingia maeneo ya misitu na kufanya uharibifu wa mazingira kwakuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Mkazi wa kijiji hicho Doi, Misalaba ameiomba Serikali kuendelea kufanya operesheni kwenye msitu huo kwa kuwa kilimo cha bangi kitasababisha madhara makubwa kwa jamii na kwenye vizazi vijavyo.
Nae hakimu wa mahakama ya wilaya ya Nyang’hwale, Daniel Nyange aliwataka wananchi kuachana na kilimo cha bangi na badala yake wajikite kwenye shughuli nyingine za kuwapatia kipato ikiwemo uchimbaji wa madini, kilimo cha mpunga na biashara.
Ameshauri elimu iendelee kutolewa ili wananchi waachane na kilimo cha bangi ambacho mbali na kuwaingiza kwenye matatizo ya kisheria lakini inaharibu jamii kwa kuharibu vijana wanaoingia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.



