Dar es Salaam – Kiungo na beki wa kushoto wa timu ya taifa ya Tanzania, Mohamed Hussein maarufu kama
Zimbwe Jr, ametangaza rasmi kuondoka Simba SC baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja.
Mohamed Hussein, aliyezaliwa tarehe 1 Novemba 1996, alijiunga na Simba SC mwaka 2014 na amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya klabu hiyo kwa miaka 11. Akiwa na uwezo wa kucheza kama beki wa kushoto na pia kiungo wa pembeni, Zimbwe Jr alikuwa mchezaji wa kuaminiwa na aliwahi kuvaa kitambaa cha unahodha katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Katika taarifa zake za hivi karibuni, Hussein ametangaza kuwa anaondoka Simba kwa nia ya kusonga mbele kitaaluma na kufikia malengo mapya. Chanzo kimoja cha habari kimeripoti kuwa anatarajiwa kujiunga na mahasimu wa jadi, Yanga SC, kwa mkataba wa miaka miwili – hatua inayotajwa kuwa miongoni mwa usajili wa kihistoria kwenye soka la Tanzania.
Zimbwe Jr alianza kuichezea timu ya taifa, Taifa Stars, tarehe 22 Novemba 2015, na amekuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki mashindano ya AFCON mwaka 2019 na 2023.Uhamisho wake kutoka Simba kwenda Yanga unafungua ukurasa mpya wa ushindani wa soka la Tanzania na kuongeza ladha ya Ligi Kuu kwa msimu ujao



