
Kiungo mahiri kutoka Guinea, Moussa Balla Conte, leo ametambulishwa rasmi kuwa mchezaji mpya wa Klabu ya Yanga SC akitokea CS Sfaxien ya Tunisia.
Kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii, Yanga SC imethibitisha kuipata saini ya kiungo huyo ambaye anasifika kwa uwezo mkubwa wa kukaba, kupiga pasi za mwisho, pamoja na kusaidia safu ya ulinzi na ushambuliaji.Usajili wa Conte ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga, kwani unaongeza nguvu mpya katika kikosi kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani na ya kimataifa, hasa katika harakati za kutetea mataji ya ligi na kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF.
Hata hivyo, usajili wake uliwahi kuibua sintofahamu kubwa, huku ripoti zikidai kuwa alikuwa mbioni kujiunga na mahasimu wao wa jadi, Simba SC. Taarifa hizo zilieleza kuwa Conte alikuwa karibu kutua Msimbazi, jambo lililozua mijadala mikubwa mitandaoni. Hata hivyo, Yanga SC imeweka mambo hadharani kwa kumtambulisha rasmi kiungo huyo, na hivyo kuweka mwisho wa tetesi zote.Conte sasa ni mali ya Wananchi, na mashabiki wa Yanga wana kila sababu ya kuwa na matumaini makubwa kwa msimu ujao kutokana na saini hii ya kimkakati.



