Kila mtu anataka kufanikiwa, hakuna asiyetaka kufanikiwa lakini kuna vitu unatakiwa kuvijua kabla ya kuanza harakati zako za kufanikiwa.
Ndiyo!
Huwezi kufanikiwa kama hutovijua hivi vitu vichache kwanza. Ni lazima vikae kichwani mwako na vikuongoze maisha yako yote.
1. TAFUTA NJIA
Hiki ni kitu cha kwanza ambacho unatakiwa kukifanya. Una mipango kabambe, tena mikubwa lakini ni lazima utafute njia sahihi ya kukifikia kitu hicho unachokitaka.
Unapotoka Kariakoo kwenda nyumbani kwenu Mbagala, huwa kuna njia nyingi za kufika huko kwenu, unataka kuchagua njia gani? Kuna ya haraka na ile ndefu. Unapochagua njia sahihi ya kupita ili ufike unapokwenda ndiyo hata kwenye mafanikio kupo hivyo.
Wewe unahitaji milioni 100 kwenye akaunti, nami pia nahitaji. Kila mmoja ana njia zake za kuipata hiyo pesa. Unaweza kuwahi kuipata kabla yangu ama mimi nikawahi, inategemea na njia tutakazopitia kuzipata pesa hizo.
2. JUST FOCUS
Hiki ni kitu muhimu sana tunachotakiwa kufanya. Tufocus kwa kile tunachokitaka. Unapotoka nyumbani kwenu na kwenda dukani kununua nguo, huwa hutakiwi kupitia sehemu yoyote ile, weka focus yako kwenye njia ya kwenda dukani na ununue nguo yako.
Sasa kwenye hili suala la mafanikio, watu hawataki kufocus. Mfano unamuuliza Nyemo unataka nini? Atakujibu niwe na App, muda huohuo atakwambia nataka niwe na Youtube channel, hujakaa sana atakwambia nataka niwe natengeneza filamu.
Ni mtu mmoja, ana malengo matatu na kitakachotokea baada ya hapo ni kupoteza focus ya jambo moja. Huwezi kufanya mambo matatu kwa wakati mmoja. Unamtuma mtoto kiberiti dukani, anakutana na mbwa na kuanza kumkimbiza, anapoteza focus, mwisho wa siku anachelewa kukuletea kiberiti.
Kitu kinachokupotezea focus yako ndicho kitakachokuchelewesha kupata jambo unalolitaka. Ukiamua kutaka kitu fulani, hebu kifocus hicho kwanza, hata kikija kingine, achana nacho, wewe endelea kukitazama kile ukitakacho mpaka kitimie.
3. HUWEZI KUFANYA PEKE YAKO
Hili ni jambo muhimu sana unalotakiwa kulifahamu. Unapoanza kufanikiwa, ni lazima ujue kwamba huwezi kufanya peke yako. Ni kweli unaweza kuanzisha kampuni peke yako lakini jua utahitaji timu.
Hii timu ndiyo itakayotakiwa kukufikisha huko unapotaka kwenda. Kuna mambo mengi yatakuibukia, hutoweza kuyasolve peke yako, ni lazima kuwe na watu ambao watakusaidia kufikia malengo. Ndiyo maana hata matajiri waliofanikiwa, walihitaji watu wa kupambana nao. Ukiwapata, watengenezee mazingira ya kutambua kwamba wewe ndiye BOSI.
4. HAKIKISHA UNA NDOTO KUBWA
Hiki ni kitu cha muhimu sana kukifanya, hakikisha unaweza ndoto yako kwenye kitu kikubwa. Mfano nikisema ndoto yangu ni kununua baiskeli, nguvu nitakayoitumia ni ya kununua baiskeli tu, sitotumia nguvu ya kutaka kununua gari.
So unatakiwa uwe na ndoto kubwa. Mimi ndoto yangu ni kununua BMW6, nafanya kazi kubwa kuhakikisha naipata hiyo gari. Nguvu ninayoifanya ni ya BMW6 lakini ikitokea siku nikaikosa gari hiyo, basi nitapata Harrier Tako la Nyani. Ila ningesema niweke ndoto kwenye Harrier, basi siku ambayo ningeikosa, ningenunua IST.
So ni lazima uweke ndoto ya kupata kitu kikubwa.
5. ACHA VISINGIZIO
Hili tunakutana nalo watu wengi, wakati tunapambania ndoto zetu tunakuwa na visingizio vikubwa na vyote huwa hatutaki kujilaumu sisi wenyewe, tunawalaumu wengine. Yaani kutokufanikisha ndoto zetu ni kwa sababu ya watu fulani.
Mtoto hajafua nguo zake, ukimuuliza kwa nini, anasema maji yalikatika. Kwa hiyo anataka mimi niwafuate Dawasco na kuwauliza kwa nini mlikata maji mpaka mtoto wangu hajafua?
Yaani tukishindwa kufanikisha kitu fulani, tunaleta visingizio kwa watu wengine, tunataka kuwaonyesha watu kwamba hatujafanya hili kwa sababu ya fulani. Sasa kwenye safari ya mafanikio yako acha visingizio. Simama wewe kama wewe, mwisho wa siku ujilaumu mwenyewe.
6. NO OTHER OPTION
Hiki ni kitu muhimu sana unachotakiwa kukijua. Yaani kaa na kusema kuwa tegemeo langu lipo kwenye kusakata kabumbu, hakuna njia nyingine yoyote ile, nikifeli hapa, ndiyo nimefeli maisha.
Ukiangalia muvi ya Rise, Giannis Antetokounmpo alimwambia mama yake kwamba hakuna jia nyingine ya kufanikiwa zaidi ya kucheza mchezo wa basketball, yaani akishindwa hapo, inamaanisha amefeli maisha.
Wakati nazungumza na rafiki yangu mmoja nilimwambia Application ndiyo my last option. Yaani hakuna zaidi ya hapo na ikitokea nimeshindwa kwenye hilo, inamaanisha nimeshindwa maisha. Inamaanisha nimefeli milele.
Kwa nini tunafanya hivyo?
Ni kwa sababu ya kupambana zaidi, hii inakupa ari kubwa ya kujitoa kwa ajili ya jambo hilo. Hakuna mtu aliyefeli baada ya kulisema hili kwa sababu kinachofuata baada ya hapo ni kujitoa kwa nguvu zote.
Ukiwa na machaguo mengi, hutoweza kufanikiwa. Manake utasema nikishindwa kwenye mpira, nitakwenda kwenye muziki. Huwezi kupambana kwa kuwa tayari ushaweka option ya pili. Hebu jiambie kwamba hakuna option ya pili, una moja tu ambayo unatakiwa kuipambania kwa nguvu kubwa.
7. SIMAMIA MALENGO YAKO
Hili ni jambo la saba na la msingi sana. Simamia malengo yako. Kuna mtu anakwambia malengo yangu ni kujenga nyumba moja kubwa na nzuri, acha nijichange.
Wakati umefikia muda wa kununua matofali, unaanza kuambiwa kuna mgonjwa anaumwa kishenzi, anahitaji kiasi kikubwa cha pesa. Bro! Simamia malengo yako. Kaanze ujenzi.
Hili ndilo wanalolifanya matajiri. Wanakuwa na pesa, wameziwekea malengo yao, halafu ghafla unaibuka na kuanza kumuelezea matatizo yako, anakwambia sina, unashangaa inakuwaje hana? Anayo ila ameweka malengo yake kwanza, hiyo pesa unayoitaka, kuna malengo ameiwekea na lazima ayatimize kwanza. Hapo ndipo sisi masikini tunaanza kuwaona matajiri wabaya.
8. TIMIZA SHAUKU YAKO
Hii inamaana ya kuufurahisha moyo wako. Unataka nini sasa hivi? Hebu ufurahishe moyo wako. Tatizo hatutaki kuifurahisha mioyo yetu na mwisho wa siku tunafuata maneno ya watu.
Shauku yako ni kununua gari. Yaani unajisemea nikipata pesa tu, nanunua gari, naamini nitakuwa na furaha. Wakati umepata pesa, kuna mtu anajitokeza na kukwambia nenda kajenge, hakuna baba mwenye gari.
Kwa sababu unaambiwa tena kwa mifano mingi, sasa unashindwa kuupa moyo wako furaha unakwenda kuanza ujenzi, yaani unafanya kitu ambacho hakikupi furaha. Ulipambana sana ili upate pesa na ununue gari, kwa nini kwanza usiupe moyo wako furaha?
Hakuna kitu kinachofurahisha kama kusema napambana ninunue kitu fulani halafu na kweli unakuja kukinunua. Furahisha moyo wako na achana na shauku za wengine

