
Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, leo Machi 26, 2026 itashuka dimbani kuivaa Liechtenstein katika michuano ya FIFA Series 2026 inayoendelea jijini Kigali, Rwanda.
Mchezo huo ni sehemu ya mashindano ya timu nne yanayozishirikisha pia Aruba na Macau, ambapo timu hizo zinakutana katika eneo moja kucheza mechi za kirafiki wakati wa dirisha la kimataifa.
Michuano ya FIFA Series ni mashindano maalumu ya mechi za kirafiki yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), yakilenga kuzikutanisha timu za mataifa ambazo mara nyingi hazipati nafasi ya kucheza pamoja.
Katika ushiriki wake wa mwisho, Taifa Stars ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Bulgaria kabla ya kurejea na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mongolia.
Kocha mkuu wa Stars, Miguel Gamondi, amesema ataitumia michuano hiyo kujenga kikosi imara kitakachoshiriki AFCON 2027 huku akilenga kupata matokeo chanya.




