
. Tanzania imedhamiria kujenga daraja litakalounganisha bara na Visiwa vya Zanzibar ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu, ambalo endapo litafanyika daraja hilo la kilomita 50 litakuwa la kwanza barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Godfrey Kasekenya Bungeni leo Aprili 28, na kuongeza kuwa mazungumzo yaliyoanza Machi 11, 2023 yako katika hatua za mwisho.
Kasekenya alisema kuwa pande hizo mbili zimekutana na wawekezaji watarajiwa wa Kampuni ya M/S China Overseas Engineering Group (COVEC) ambao wameonyesha nia ya kujenga daraja hilo.
Amesema matokeo ya kikao hicho bado yanafanyiwa kazi na pande zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar huku akibainisha kuwa mpango wa ujenzi wa daraja hilo utahusisha ushirikiano na sekta binafsi.
Alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mwantum Dau Haji (CCM Viti Maalumu) aliyetaka kujua ni lini ujenzi wa daraja hilo utaanza.
Wazo la daraja hilo lilikuja kwa mara ya kwanza mwaka 2020 wakati baadhi ya Watanzania wanaoishi ughaibuni walipoanzisha mpango wa ujenzi wa daraja la bahari litakalounganisha kisiwa cha Unguja na Dar es Salaam.
Wazo hilo lilizua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi huku wengine wakisema kuwa ni ndoto ya mchana. Lakini sayansi na teknolojia imethibitisha kuwa mradi wa kujenga takriban kilomita 50 za Daraja la Zanzibar/Dar es Salaam unawezekana iwapo fedha zinapatikana.



