
Tanzania imepanda kwa nafasi moja katika chati ya viwango vya ubora vya nchi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kulingana na mafanikio ya klabu kwenye mashindano ya Afrika.
Chati hiyo inatokana na tathmini ya ushiriki wa miaka mitano wa klabu za nchi husika katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
Tanzania ambayo ilikuwa nafasi ya sita, sasa ipo nafasi ya tano huku Tunisia iliyokuwa nafasi ya tano ikishuka hadi ya sita.
Kupanda kwa Tanzania kumetokana na kukusanya idadi ya pointi 82.5 katika kipindi cha misimu mitano iliyopita ya ushiriki wa klabu zake katika mashindano ya klabu Afrika.
Idadi kubwa ya pointi kwa Tanzania imekusanya msimu uliopita ambao imekusanya jumla ya pointi 30.
Pointi 20 imezipata kutokana na Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na pointi 10 imevuna kwa Yanga kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Chati hiyo inaongozwa na Misri ambayo ina pointi 190.5, huku nafasi ya pili ikiwa Morocco yenye pointi 142.


