

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Jana Februari 08, 2026 amezindua soko jipya la Kariakoo lililopo Ilala jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alishiriki katika uzinduzi huo ambapo amesema kuwa uamuzi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia wa ujenzi wa soko hilo, ni ishara ya dhati ya kujitoa kwake kwa Watanzania, hususan wafanyabiashara wa Kariakoo na watumiaji wa soko hilo.
Amesema Rais Dkt. Samia ameendelea kurejesha tabasamu kwa wananchi kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi anazozitoa, jambo linalodhihirisha uongozi wake wa vitendo na unaojali maslahi ya watu.
Ameeleza kuwa soko hilo limejengwa kwa misingi ya kisasa, kwa kuzingatia maono ya Rais Samia, ili kuhakikisha mazingira salama na rafiki kwa wafanyabiashara.
Amesema kuwa soko hilo limewekewa mifumo imara ya umeme, kamera za ulinzi pamoja na jenereta za dharura, hatua zinazolenga kuongeza usalama na ufanisi wa shughuli za biashara.
Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na kukuza uchumi wa wananchi kupitia miundombinu ya kisasa na endelevu.

