
Ameyasema haya
“Nimewasili nchini Korea Kusini kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Korea, Mheshimiwa Yoon Suk Yeol. Korea ni moja ya washirika wetu wakubwa wa maendeleo tangu tulipoanza nao rasmi uhusiano wa kidiplomasia tarehe 30 Aprili 1992.
Uhusiano wetu na Korea umegusa maisha ya wananchi moja kwa moja na lazima kuendelea kufanya kazi ya kuukuza na kuuongezea tija zaidi. Baadhi ya miradi mikubwa ambayo tumeshirikiana na Korea kuifanikisha ni pamoja na Daraja la Mto Malagarasi, Daraja la Tanzanite na Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila.
Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa kazi ya Diplomasia ya Uchumi, na baada ya mazungumzo kati yangu na Mheshimiwa Rais, nchi zetu zitasaini makubaliano mbalimbali ya kukuza zaidi uhusiano wetu yakigusa hasa sekta za uchukuzi, uchumi wa buluu, usafiri wa anga, madini ya kimkakati, utamaduni, sanaa na kilimo.
Baadaye nitafanya mazungumzo na viongozi wa kampuni kubwa za Korea kwenye sekta za nishati, miundombinu na uandaaji wa filamu ili kuona namna nchi zetu zinavyoweza kushirikiana kwenye maeneo haya ikiwemo kukuza teknolojia, utalii, kuwekeza katika studio za filamu nchini na ujenzi wa Chuo cha Filamu cha Taifa (Tanzania National Film Academy).
Kabla ya kuhitimisha ziara nitashiriki Jukwaa la Afrika na Korea (Korea-Africa Summit) linalowaleta pamoja Wakuu wa Nchi za Afrika na Serikali ya Korea. Nitahutubia jukwaa hilo na kushirikishana uzoefu na mikakati katika usalama wa chakula na madini.”



