Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bw. Emmanuel Tayari, kusimamia kwa karibu shughuli zote za ujenzi na uendelezaji wa viwanda vya dawa nchini pamoja na wawekezaji wake, ili ifikapo mwaka 2030 Tanzania iweze kujitegemea kwa angalau asilimia 80 katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo, Februari 9, 2026, wakati wa hafla ya uapisho wa viongozi iliyofanyika katika Ikulu , Jijini Dar es Salaam, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji katika sekta ya viwanda vya dawa.”
“Najua unaweza kusimamia viwanda vya dawa na wawekezaji. Nenda kasimamie, nenda ukaelewe wanaowekeza ni kina nani. Watu wengi wana hamu ya kuja kuwekeza lakini wanakwazwa na masuala ya ardhi pamoja na ukiritimba wetu. Nataka ukasimame kuhakikisha viwanda vya dawa vinajengwa ndani ya nchi yetu, na ifikapo 2030 tujitegemee kwa si chini ya asilimia 80,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amemtaka Bw. Tayari kuhakikisha anasimamia kikamilifu mchakato mzima wa ujenzi wa viwanda vya dawa, kuondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha uwekezaji, na kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje, ili Tanzania iweze kuongeza uzalishaji wa dawa zinazotengenezwa nchini na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.



