
Mapema leo katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa (National Defense College) ambapo nimetoa mhadhara kuhusu matumizi ya R Nne kwa washiriki wa Kozi ya 12 ili kusaidia katika uongozi, uchumi, ustawi, ulinzi na usalama wa taifa letu.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011, dira ya chuo chetu cha Ulinzi cha Taifa ni kuwa sehemu ya mafunzo bora kwa Maafisa Wakuu wa Jeshi ndani ya nje ya nchi, vyombo vya usalama na watumishi wa umma katika nyanja ya usalama na stratejia, eneo ambalo ni msaada mkubwa katika kutunga na kutekeleza sera zinazosimamia uwepo na ustawi wa nchi yetu na watu wake.
Nimewashirikisha washiriki mtazamo na uzoefu wangu kwenye utekelezaji na matokeo ya Falsafa ya R Nne yenye misingi mikuu ya:- Reconciliation (Maridhiano pale tunapokinzana), Resilience (Ustahamilivu pale tunapotofautiana), Reform (Mabadiliko pale ambapo hatuna budi kufanya hivyo ili kusonga mbele na kuwa bora zaidi) na Rebuilding (Kujenga Upya ili kutoka tulipo na kwenda mbele).
Imani yangu ni kuwa baada ya kuhitimu mafunzo, washiriki watakwenda kuwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa maono ya nchi yetu na nchi zao (kwa washiriki toka mataifa ya nje), katika kuendelea kujenga misingi ya mataifa yetu ili kupiga hatua bora zaidi kwenda mbele kufikia malengo na matarajio ya wananchi wetu.



