Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya STANBIC ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Patrick Rutabanzibwa, akiwa ameambatana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Manzi Rwegasira, pamoja na Mkuu wa Huduma za Sheria, Bw. Eric Rwelamira, ambapo walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta ya benki ili kuongeza mchango wa sekta ya fedha katika kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha uwekezaji na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha zinazounga mkono maendeleo ya Taifa.
Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili pia kuhusu mikakati ya Benki ya STANBIC ya kuendelea kushiriki kimkakati katika sekta mbalimbali za uzalishaji, sambamba na kuunga mkono Dira ya Tanzania ya kufikia uchumi wa thamani ya dola za Marekani Trilioni 1 ifikapo mwaka 2050 ambapo Benki hiyo ilieleza utayari wake wa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa suluhisho bunifu za kifedha, kuvutia uwekezaji na kuwezesha ukuaji wa sekta binafsi, hatua zinazotarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya uchumi wa nchi.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kamishn awa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha.
