
Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ametoa tuzo kwa washindi wa Shindano la Masoko ya Mitaji kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu, pamoja na vyeti kwa wahitimu wa mafunzo ya watendaji katika masoko ya mitaji wanaokidhi viwango vya kimataifa, katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jijini Dar es Salaam..
Mhe. Balozi Omar alisema Serikali inaendelea kutekeleza Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21–2029/30, unaolenga kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za fedha.

Alibainisha kuwa mafanikio yameanza kuonekana, ambapo hadi Desemba 2025, thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji na dhamana imefikia shilingi trilioni 63.15, huku mauzo ya hisa na hatifungani yakifikia shilingi trilioni 6.9.
Aidha, Serikali inatarajia kutumia sekta ya masoko ya mitaji kama njia muhimu ya kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo na kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wao, sambamba na utekelezaji wa DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aliipongeza CMSA kwa mikakati ya ubunifu iliyopelekea kuzinduliwa kwa bidhaa saba muhimu za kifedha, ikiwemo Hatifungani za Kijani, Hatifungani za Kijinsia (NMB Jasiri Bond), Hatifungani za Jamii (NMB Jamii Bond) na Sukuk zinazozingatia misingi ya Shariah, ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kugharamia miradi ya maendeleo nchini.
Mhe. Balozi Omar pia alisifu ushiriki mkubwa wa wanafunzi 28,393 katika shindano la masoko ya mitaji, idadi iliyovuka lengo lililowekwa la washiriki 20,000, sawa na mafanikio ya asilimia 142.

Alisema kuwa shindano hilo limeiweka Tanzania katika ramani ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kama nchi ya mfano katika elimu ya masoko ya mitaji kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Vilevile, Mhe. Balozi Omar aliwapongeza wahitimu 95 wa mafunzo ya watendaji wa masoko ya mitaji, waliopata mafunzo yanayotambuliwa kimataifa kupitia ushirikiano wa CMSA na taasisi ya Chartered Institute for Securities and Investment (CISI) ya London, akisisitiza kuwa wahitimu hao watasaidia kuongeza weledi na ushindani katika sekta ya masoko ya mitaji nchini.

Waziri alihitimisha kwa kuhimiza CMSA na wadau wake kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masoko ya mitaji, kuimarisha mifumo ya kushughulikia malalamiko ya wateja kwa wakati, na kuhakikisha kanuni na sheria za masoko ya fedha zinazingatiwa ipasavyo.
“Masoko ya mitaji ni injini ya ukuaji wa uchumi wa kisasa. Ni imani yangu kuwa ninyi mliopata vyeti leo mtakuwa chachu ya maendeleo katika sekta hii muhimu,” alisema Waziri Omar kabla ya kukabidhi tuzo na vyeti kwa washindi na wahitimu.

Kwaupande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, alisema kuwa Mamlaka itaendelea kuhamasisha ubunifu na ujenzi wa weledi katika sekta ya masoko ya mitaji ili kuongeza ushiriki wa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Alisema mashindano hayo ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa jukumu la CMSA la kuelimisha umma kuhusu masoko ya mitaji na kujenga uwezo wa wataalamu kwenye sekta hiyo.

CPA Mkama alifafanua kuwa shindano hilo linahusisha sehemu mbili kuu: shindano la maswali na majibu (Quiz Competition) na shindano la uandishi wa insha (Essay Competition), likiwa na lengo la kujenga uelewa wa uwekezaji na matumizi ya masoko ya mitaji miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.
“Washiriki 89 waliopata alama za juu walitambuliwa, na miongoni mwao washindi wa juu 12 (wavulana 6 na wasichana 6) watapata fursa ya ziara ya mafunzo nchini Nigeria. Washindi wa nafasi tatu bora walizawadiwa fedha kati ya shilingi milioni tatu na laki tano, huku washiriki wote wakipewa vyeti, fulana, na kofia zenye nembo ya CMSA” alisema CPA Mkama.

Alisema kuwa CMSA imeweka utaratibu wa kuwahamasisha washindi kuwa wawekezaji halisi kwa kuwekeza theluthi moja ya zawadi ya tuzo zao katika hisa au mifuko ya uwekezaji ya pamoja.
Alitaja mfano wa washiriki wa miaka iliyopita waliowekeza shilingi milioni 10, ambazo sasa zimeongezeka hadi kufikia zaidi ya shilingi milioni 125, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 1,100.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dkt. Yamungu Kayandabila; Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Lucas Mwimo; Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA. Nicodemus Mkama; na wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, na taasisi za fedha nchini.






