
Klabu ya Simba SC imeingia hatua mpya ya mageuzi baada ya kuzindua rasmi mpango wa utoaji wa kadi mpya za uanachama zitakazokuwa na mfumo wa kisasa wa kifedha, ambapo kadi hizo zitafanya kazi kama VISA Card. Hatua hii inalenga kuongeza urahisi wa miamala, usalama wa fedha na kuimarisha uanachama wa klabu kwa viwango vya kimataifa.
Tangazo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Crescentius Magori, wakati wa hafla maalum ya kutambulisha ushirikiano kati ya Simba, Mainstream Group pamoja na Nexus Pesa.
Mainstream na Nexus Wachaguliwa Kutengeneza Kadi
Akizungumza mbele ya wanahabari, Magori amesema bodi imefanya utafiti wa kina kutafuta kampuni yenye uwezo mkubwa wa kutengeneza kadi za kisasa zinazolingana na hadhi ya klabu kubwa barani Afrika.
“Leo tumekusanyika hapa kwa jambo la muda mrefu ambalo limesubiriwa sana. Tulikuwa tunatafuta kampuni ya uhakika kutengeneza kadi za Simba, kadi za uanachama ambazo zinafanana na timu kubwa kabisa Afrika,” alisema Magori.
Ameongeza kuwa kampuni ya Mainstream Group ndiyo imepewa dhamana ya kutengeneza mfumo wa kadi hizo, huku Nexus Pesa ikipewa jukumu la kuzitoa kwa wanachama.
“Bodi ya Wakurugenzi inapenda kuitangaza kampuni ya Mainstream kuwa ndiyo itatengeneza kadi za mfumo wa kileo na za kisasa na imeichagua kampuni ya Nexus kutoa kadi hizi za wanachama. Kadi hizi zitakuwa aina ya VISA,” aliongeza.
Kadi Zitakuwa na Huduma za Kibenki
Moja ya faida kubwa za kadi hizi mpya ni uwezo wake wa kufanya kazi kama kadi ya benki, kuruhusu wanachama kufanya miamala ya kifedha ikiwemo kuweka fedha, kulipia huduma mbalimbali na kufanya malipo kwa njia ya kidigitali.
“Hii itakuwa Visa card, pamoja na kukutambua kwamba ni mwanachama wa Simba lakini pia unaweza kuweka pesa, ukafanya malipo na miamala mbalimbali,” alisema Magori.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza urahisi wa huduma kwa wanachama, pamoja na kuifanya Simba kuwa miongoni mwa klabu za kwanza Afrika Mashariki kuanzisha mfumo wa kadi za uanachama zenye huduma za kifedha.
Usajili wa Matawi Kuanza Hivi Karibuni
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu, amesema mpango wa utoaji wa kadi hizi utafuata taratibu zote zilizopo ndani ya Katiba ya Simba kuanzia ngazi ya matawi hadi makao makuu.
“Tumeingia mkataba na wenzetu Mainstream Group na Nexus Pesa, utoaji wa kadi za uanachama utafata katiba ya Simba kuanzia ngazi ya matawi hadi ngazi ya makao makuu ya klabu. Ni wakati muafaka kwa wanachama hasa kwenye ngazi ya matawi na tutaanza usajili wa matawi hivi karibuni,” alisema Mangungu.
Tarehe Rasmi ya Kuanza Kutolewa kwa Kadi
Mangungu amebainisha kuwa zoezi rasmi la kutoa kadi hizi kwa wanachama litaanza tarehe 27 Machi 2026, baada ya maandalizi ya kina yanayohusisha taasisi mbalimbali kukamilika.
“Tumepanga kuanza kutoa kadi tarehe 27 Machi 2026. Tunafanya hivyo kwa sababu kuna mambo mengi ya kiufundi na taasisi nyingi zinazohusika katika maandalizi ya utoaji wa hizi kadi,” alisema.
Hatua Kubwa kwa Mageuzi ya Simba
Uzinduzi wa kadi hizi mpya unatajwa kuwa hatua kubwa katika safari ya mageuzi ya Simba SC, yenye lengo la kuifanya klabu kuwa ya kisasa, yenye mifumo ya kimataifa na inayotoa huduma bora kwa mashabiki na wanachama wake.
Kwa mfumo huu mpya, wanachama wa Simba wanatarajiwa kunufaika na urahisi wa huduma, usalama wa miamala, pamoja na fursa mbalimbali za kibiashara zitakazotokana na matumizi ya kadi hizo.


