
Klabu ya Young Africans SC imepoteza mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco, matokeo yanayofanya hatima ya kufuzu hatua ya robo fainali kusubiri mpaka mchezo wa mwisho wa Kundi B.
Katika mchezo huo uliochezwa nchini Morocco, Yanga ilijitahidi kupambana lakini ilishindwa kupata bao la kusawazisha baada ya wenyeji AS FAR kutumia vyema nafasi waliyoipata na kuondoka na pointi zote tatu.
Katika mchezo mwingine wa Kundi B, mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri walitoka sare tasa ya 0-0 dhidi ya JS Kabylie. Matokeo hayo yameifanya Al Ahly kujihakikishia tiketi ya kufuzu hatua ya robo fainali ikiwa na alama 9.
Baada ya michezo hiyo, msimamo wa Kundi B unaonesha Al Ahly kileleni wakiwa na alama 9, wakifuatiwa na AS FAR wenye alama 8, Yanga ikiwa na alama 5, huku JS Kabylie ikishika mkia kwa alama 3.
Kwa hali hiyo, Yanga italazimika kushinda mchezo wake wa mwisho dhidi ya JS Kabylie na kusubiri matokeo ya mchezo kati ya Al Ahly na AS FAR ili kujua hatima ya kusonga mbele au kuaga mashindano hayo.
Michezo ya mwisho ya Kundi B itachezwa tarehe 15 Februari 2026, ambapo Al Ahly watavaana na AS FAR, huku Yanga wakimenyana na JS Kabylie katika mechi zitakazoamua hatima ya timu zitakazofuzu robo fainali.
Matarajio ya mashabiki wa Yanga yamesalia katika ushindi wa lazima dhidi ya JS Kabylie, huku wakitarajia matokeo yatakayowapa nafasi ya kuendelea na safari yao ya kimataifa.



1 thought on “Yanga Yapoteza Ugenini Dhidi ya AS FAR, Hatima ya Robo Fainali Yasubiri Mechi ya Mwisho”