
Serikali Yafafanua Hatua za Kudhibiti Mikopo Yenye Riba Kubwa
Dodoma – Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza kuwa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti mikopo yenye riba kubwa, kwa lengo la kuwalinda wananchi dhidi ya mikopo hatarishi, ikiwemo kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Mhe. Nyakisa Sanga, aliyekuwa akiuliza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha wananchi, hususan wafanyakazi, hawabebeshwi mzigo wa riba kubwa za mikopo.
Usimamizi wa Taasisi za Fedha
Mhe. Munde amesema Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kusimamia kwa karibu taasisi za fedha ili kuhakikisha zinazingatia sheria, kanuni na miongozo ya utoaji wa mikopo nchini.
Akijibu swali la msingi kuhusu uwezekano wa riba za mikopo kwa wafanyakazi kupunguzwa na kufikia kati ya asilimia 7 au 8, Naibu Waziri amesema kuwa kwa mujibu wa sera za uchumi wa nchi, viwango vya riba huamuliwa na nguvu za soko, hivyo Serikali haiwezi kuelekeza moja kwa moja taasisi za fedha kuweka viwango maalum vya riba kwa kundi fulani la wakopaji.
“Riba za mikopo nchini huamuliwa na soko. Serikali ikielekeza taasisi za fedha kuweka kiwango maalum cha riba kwa wafanyakazi au mkopaji yeyote, itakuwa inakinzana na mwelekeo wa sera ya soko huria,” alisema Mhe. Munde.
Uwezekano wa Riba Nafuu Kupitia Majadiliano
Mhe. Munde amefafanua kuwa taasisi za fedha zina uhuru wa kuweka viwango vya riba vya chini, ikiwemo asilimia 7 au pungufu, endapo zitaona inafaa kufanya hivyo kwa kuzingatia mazingira ya biashara.
Ameongeza kuwa wafanyakazi binafsi au kupitia waajiri wao wana fursa ya kufanya majadiliano na benki husika ili kukubaliana juu ya viwango vya riba vinavyoweza kutolewa.
Ahadi ya Serikali kwa Wananchi
Naibu Waziri amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kifedha nchini kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu na yenye tija kwa wananchi, huku ikilinda misingi ya sera ya soko huria inayotumika nchini.


