Katika Jarida la habari la Uingereza BBC, iliandikwa kuwa “binadamu wote tuna uwezo wa kuishi milele baada ya kufa. Jarida hili linaendelea kusema, “Binadamu wote tuna kitu kinachoitwa nafsi. Nafsi ni mtu wa ndani ambaye huendelea kuishi baada ya mwili kufa.”
Katika falsafa “nafsi” huelezewa kuwa utu ulio ndani ya mtu ambao humtofautisha na watu wengine. Katika theolojia au elimu ya dini, nafsi inafafanuliwa kuwa sehemu ya uungu iliyo ndani ya kila mtu ambayo huendelea kuwa hai baada ya mwili kufa. Wanafalsafa wa mapema waliamini dhana ya Kigiriki kwamba nafsi imeumbwa na Mungu na huingizwa ndani ya mwili wakati wa kutunga kwa mimba.
HISTORIA
Imani kuhusu kitu kinachoitwa “nafsi” siyo ngeni, imekuwepo sehemu mbalimbali za dunia tangu zamani hata kabla ya ujio wa dini za Ukristo na Uislamu. Wagiriki wa kale waliamini kuwa, nafsi ni asili ya uungu iliyondani yetu ambayo imekuwepo kabla yetu na huendelea kuwepo hata baada ya mtu kufa. Wamisri wa kale waliamini nafsi imegawanyika katika sehemu mbalimbali ambazo ni utambulisho wa kiroho unaotofautisha mtu na wengine. Wahindu wana imani zao juu ya nafsi, wabudha vilevile na karibu kila dini kubwa na ndoto ulimwenguni huamini juu ya kitu ambacho huendelea kuishi baada ya mtu kufa.
UPAGANI
Kwa mujibu wa ukurasa wa kamusi ya mtandao Wikipedia, Upagani ni neno linalotumika kutaja imani za dini zote zinazoabudu miungu mingi au kufuata imani za jadi. Kamusi ya Kiswahili huelezea Upagani kama hali ya kufuata dini za kienyeji zisizo na maandiko matakatifu kama vile Biblia au Kurani. Dini zinazodai kuabudu Mungu mmoja hupinga vikali imani za kipagani, lakini linapokuja suala la kutokufa kwa nafsi dini zote huungana na kuzungumza lugha moja. Dini zote pamoja na wapagani kwa ujumla, huamini uwepo wa nafsi isiyoweza kufa.
SAYANSI INASEMAJE
Baada ya tafiti zilizodumu kwa miongo kadhaa kugonga mwamba, tafiti zilizojikita kuchunguza jinsi wagonjwa mbalimbali walivyokuwa wakifariki, ili kutafuta ushahidi wa kisayansi ambao ungeonyesha namna nafsi zao zilivyoacha mwili, tafiti hizo zilisitishwa rasmi na kutupiliwa mbali. Majibu yaliyotolewa ni kwamba, sayansi haitambui uwepo wa kitu kiitwacho nafsi wala haikubaliani hata kidogo na madai ya dini kuwa binadamu wana nafsi ambayo hutengana na mwili na huendelea kuishi mtu anapokufa. Kisayansi imethibitishwa kuwa hakuna kiashiria chochote kinachothitisha jinsi nafsi inavyotengana na mwili, wala hakuna sehemu ya mwili ambayo huendelea kuwa hai baada ya kifo.
REINCARNATION
Hii ni imani kuwa mtu anapokufa nafsi au roho yake huzaliwa upya katika mwili mwingine kwa kuchukua umbile la kibinadamu, mnyama au roho ikitegemea kiwango cha ubora wa matendo yake kabla ya kifo chake. Ukristo na Uislamu haukubaliani na imani hii.
HITIMISHO
Mwanafalsafa kutoka Ufaransa Descartes aliwahi kusema, “akili na mwili ni vitu viwili tofauti, hii inamaanisha akili ndiyo nafsi.” Jiulize, ikiwa akili ndiyo nafsi, ni nini hutokea akilini baada ya mtu kufa? Je, huu ni ushahidi kwamba nafsi huharibika mwili unapokufa?
Wachunguzi wa mambo huainisha kuwa nafsi siyo kitu kilicho ndani ya mwili wa kiumbe, bali nafsi ni kiumbe huyo mwenyewe. Hii inamaanisha kila kiumbe aliyehai ni nafsi hai. Hivyo, kiumbe hai anapokufa, nafsi au thamani yake huhesabika kuwa mfu yaani nafsi iliyokufa.



